Ufufukaji wa uchumi wa China kunufaisha uchumi wa dunia unaokabiliwa na changamoto
2023-04-20 15:08:12| CRI

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) hivi karibuni lilitoa ripoti, likipunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi wa nchi kubwa kiuchumi duniani, isipokuwa China, ambayo uchumi wake unakadiriwa kukua kwa asilimia 5.2 kwa mwaka huu. Kabla ya hapo, Benki ya Dunia pia ilitoa makadirio yake ya ukuaji wa uchumi wa China. Rais wa Benki hiyo David Malpass amesema uchumi wa dunia utakuwa dhaifu mwaka huu, lakini uchumi wa China utakuwa wa "kipekee."

Ripoti ya IMF sio tu ilipunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka huu hadi asilimia 2.8, bali pia ilitumia maneno mazito kama vile “changamoto kubwa”, “utatanishi” na “hatari” kuelezea hali ya uchumi wa dunia. Ripoti hiyo inakadiria kuwa mwaka huu, ukuaji wa mapato ya nchi nyingi utapungua, na kiwango cha ukosefu wa ajira kitaongezeka, wakati huohuo ukuaji wa uchumi kwa takriban asilimia 90 ya nchi zilizoendelea utapungua. Ripoti hiyo pia ilitaja sababu kuu ambazo ni pamoja na msukusuko wa mambo ya kifedha katika nchi za magharibi, mfumuko wa bei, mgogoro unaoendelea nchini Ukraine, na athari ya janga la COVID-19.

Kutokana na hali ngumu duniani, uchumi wa China umeendelea kuonyesha mwelekeo wa kufufua. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Idara Kuu ya Takwimu ya China, pato la taifa la China katika robo ya kwanza ya mwaka huu lilikuwa dola trilioni 4.16 za Kimarekani, ambalo ni ongezeko la asilimia 4.5 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hiki, na kuzidi makadirio yaa awali ambayo ni asilimia 4.0.

Ukuaji mzuri wa uchumi wa China unatokana na msingi wake thabiti. Mwaka jana, pato la taifa la China lilifikia dola trilioni 18 za kimarekani, na kuendelea kushika nafasi ya pili duniani. Pato la taifa kwa mtu lilifikia dola 12,741 za kimarekani, thamani ya biashara ya bidhaa ilizidi dola trilioni 6.2 za kimarekani. Licha ya hayo, China ina soko kubwa mno kutokana na idadi yake ya watu ambao ni zaidi ya bilioni 1.4, na kundi la watu wenye kipato cha kati zaidi ya milioni 400. Aidha, nia thabiti ya kufungua mlango pia ni sababu muhimu ya ukuaji wa uchumi wake.

Ukuaji mzuri wa uchumi wa China umeleta matumaini kwa uchumi wa dunia. Mkurugenzi mkuu wa IMF Kristalina Georgieva hivi karibuni alisema, China inatarajiwa kuchangia takriban theluthi moja ya ukuaji wa uchumi wa dunia mwaka huu, na kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi nyingine. Mshauri wa masuala ya uchumi ambaye pia nia mkurugenzi wa idara ya utafiti ya shirika hilo Pierre-Olivier Gulancha amesema China itakuwa injini kuu ya ukuaji wa uchumi duniani.

Wachambuzi wameeleza kuwa, jumuiya ya kimataifa ina matumaini makubwa juu ya manufaa yatakayoletwa na uchumi wa China kwa uchumi wa dunia. Kwanza ni kutokana na ukubwa wa uchumi wa China. Hivi sasa uchumi cha China tayari umechukua asilimia 18 ya uchumi wa dunia, na ukuaji wake mzuri bila shaka utatoa mchango kwa ukuaji wa uchumi wa dunia. Kwa upande mwingine, China imesisitiza kufungua mlango zaidi, kwa kupitia mifumo mbalimbali ya ushirikiano kati yake na  pande nyingi ikiwemo pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Nchi za Kiarabu.

Kwa kuwa na lengo la kupata maendeleo ya pamoja na nchi nyingine duniani, ukuaji wa China hakika utanufaisha uchumi wa dunia.