China na Gabon zainua ngazi ya uhusiano
2023-04-20 08:52:26| CRI

Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Jamhuri ya Gabon Ali Bongo Ondimba ambaye yuko ziarani nchini China wamekubaliana kuinua uhusiano wa nchi hizo mbili hadi kwenye ngazi ya "wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa kina."

Kwenye mazungumzo yao ya jana Jumatano, rais Xi aliipongeza Gabon kwa  juhudi zake za kutafuta njia ya maendeleo inayolingana na hali ya nchi yake, na kutafuta utulivu wa kitaifa na uchumi mseto, na kwamba mafanikio makubwa yamepatikana katika maendeleo ya taifa. Xi pia alisema Gabon imekuwa ikikuza mchakato wa  mawasiliano ya kikanda na upatanishi wa masuala muhimu barani Afrika.

Kuhusu ushirikiano kati ya China na Afrika, Xi alisema China inapenda kutoa fursa mpya kwa nchi za Afrika kupitia maendeleo yake na kujenga ushirikiano wa kivitendo kati ya China na Afrika kuwa mfano wa ushirikiano wa Kusini na Kusini na ushirikiano wa kimataifa na Afrika.

Kwa upande wake, rais Bongo alishukuru mchango muhimu wa China katika kukuza uchumi wa Gabon na maendeleo ya kiviwanda. Alisema pande hizo mbili zinaweza kuimarisha zaidi ushirikiano katika miundombinu, kilimo na utalii. Bongo pia alisema Gabon inafuata kithabiti sera ya China moja na kuunga mkono dhana muhimu zilizopendekezwa na rais Xi, ikiwa ni pamoja na Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, Mpango wa Maendeleo ya Dunia , Mpango wa Usalama wa Dunia  na ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.