Wizara ya Afya nchini Kenya imetangaza mikakati mipya inayosisitiza ufadhili endelevu na uvumbuzi ili kutokomeza ugonjwa wa malaria itakapofika mwaka 2030.
Akizungumza jijini Nairobi na wanahabari kabla ya Siku ya Malaria Duniani hapo April 25, Katibu wa Kudumu wa Wizara hiyo Josephine Mburu amesema, Wizara hiyo inapanga kutumia vifaa vya kivumbuzi kama vile matumizi ya droni katika udhibiti wa vyanzo vya mazalia ya mbu katika kanda za maziwa zilizoathiriwa sana na ugonjwa huo.
Amesema Kenya inapanga kusambaza vyandarua milioni 18.3 vilivyowekwa dawa katika kaunti 28 zilizopangwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, na kuongeza kuwa, serikali inalenga kuhakikisha kila familia katika maeneo yanayoathiriwa zaidi na malaria zina chandarua kimoja kwa kila wanafamilia wawili, kama njia mojawapo ya kupunguza mzigo wa malaria nchini humo.