Mjumbe wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Zhang Jun ameitaka jumuiya ya kimataifa iziunge mkono nchi za Maziwa Makuu kujenga mustakabali wa pamoja.
Balozi Zhang amesema hayo katika Mkutano wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Maziwa Makuu. Amesema huu ni mwaka wa kumi tangu kusainiwa kwa Waraka wa kimfumo wa amani, usalama na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Maziwa Makuu, na kwamba jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuunga mkono nchi za sehemu hiyo kurejesha mchakato huo muhimu, ili kujenga mustakabali wa pamoja.
Balozi Zhang amesema, nchi za sehemu hiyo zinapaswa kutekeleza ahadi zao za pamoja, kutatua tofauti zao kwa njia ya mazungumzo, na kuhimiza kwa pamoja makundi yenye silaha kusitisha migogoro.
Pia amesisitiza kuwa, China inapenda kutoa misaada chini ya mfumo wa mfuko wa amani na maendeleo kati ya China na Umoja wa Mataifa, na kutarajia wenzi muhimu watachanga fedha ili kutoa misaada kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati mipya.