Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limezipongeza serikali za nchi za Afrika na wenza wake kwa kuzindua mapendekezo yanayowezesha wanawake wanaofanya biashara ya kuvuka mpaka.
Katika mkutano wa wazi wa Baraza hilo uliolenga kujadili ajenda za maingiliano ya wanawake, amani na usalama katika utekelezaji wa makubaliano ya Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA), Baraza hilo limerejea tena nafasi muhimu ya wafanyabiashara wanawake katika kuondokana na umasikini wa kifamilia.
Hata hivyo, Baraza hilo limeeleza wasiwasi wake kuwa kipato kinachotokana na fursa za kiuchumi katika biashara isiyo rasmi ya kuvuka mpaka kwa wafanyabiashara wanawake inakabiliwa na tishio la kurudishwa nyuma kutokana na mapigano kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.