Qin Gang: Ardhi ya China iliyorudishwa kamwe haitapotea tena
2023-04-21 15:46:41| cri

Mjumbe wa taifa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Qin Gang amesisitiza kuwa, suala la Taiwan ni kiini cha maslahi makuu ya China, na China kamwe haitaruhusu na wala haitavumilia nchi yoyote au mtu yeyote kukiuka kanuni ya China Moja na kuharibu mamlaka na usalama wa taifa la China, na ameonya kuwa yeyote atakayechezea moto kwenye suala la Taiwan, hakika atajiunguza.

Bw. Qin Gang amesema hayo alipohudhuria Jukwaa la Lanting kuhusu “ujenzi wa mambo ya kisasa wenye umaalumu wa China na dunia” lililofanyika Aprili 21 mjini Shanghai. Bw. Qin amesema tangu kale hadi leo Taiwan siku zote ni sehemu isiyotengeka ya China, na kando mbili za mlango bahari wa Taiwan zote ni ardhi ya China, hii ni historia ya Taiwan na pia ni hali ya sasa ya Taiwan. Amesema, Taiwan kurudi kwa China ni sehemu ya utaratibu wa kimataifa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambayo imewekwa wazi kwenye Azimio la Cairo (Cairo Declaration) na Taarifa ya Potsdam (Potsdam Declaration). Amesema wale wanaokiuka kanuni za kimataifa, kubadilisha hali ya sasa kwa upande mmoja na kuvuruga utulivu wa eneo la Taiwan, hawatokei China Bara, bali ni wafarakanishaji wa Taiwan na nchi chache zinazojaribu kutumia suala la Taiwan kujitafutia maslahi ya kisiasa. Bw. Qin Gang amebainisha kuwa lengo lao ni “kuifarakanisha China” kwa njia ya amani, kubadilisha historia ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kupindua utaratibu uliopo wa kimataifa baada vita hiyo, na kupuuza mamlaka ya taifa la China, na Wachina bilioni 1.4 kamwe hawatakubali.