Mnadhimu Mkuu wa rais wa mpito wa Mali auawa katika shambulizi
2023-04-21 10:05:39| CRI

Mnadhimu Mkuu wa ofisi ya rais wa mpito wa Mali, Adjudant Oumar Traore aliuawa katika shambulizi la kuvizia kusini magharibi mwa Mali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Mali, shambulizi hilo lililenga ujumbe wa kazi za kijamii wa rais wa mpito, ambapo watu wanne waliuawa, akiwemo Bw. Traore.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu ni lini shambulio hilo lilitokea au nani alihusika.

Tangu mwaka 2012, Mali imekuwa ikikumbwa na uasi, uvamizi wa wanajihadi, na ghasia kati ya jamii ambazo zimesababisha maelfu ya watu kuuawa na mamia ya maelfu kukimbia makazi yao.