Watoto watatu kati ya 10 Tanzania wapo hatarini kupata kisukari
2023-04-23 20:47:27| cri

Ripoti ya Utafiti wa Afya, Viashiria na Malaria iliyotolewa nchini Tanzania imesema, watoto wenye umri kati ya miezi sita hadi miezi 23 nchini humo na duniani kwa ujumla, wapo hatarini kupata ugonjwa wa kisukari kutokana na kubadilika kwa mtindo wa maisha na malezi.

Ripoti hiyo ya mwaka 2022 iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) nchini Tanzania, imeonesha kuwa kundi hilo lipo hatarini kwa sasa kupata kisukari na kuongeza uzito uliopitiliza.

Daktari Zainabu Hussein wa Kituo cha Afya cha Shirika la Reli (TRC) mjini Dodoma, Tanzania, amesema mtoto katika umri huo ana uwezekano wa kupata kisukari endapo akitumia vinywaji vyenye sukari kupita kiasi.