Viwanda vidogo 500 vya Wachina vimewekezwa Tanzania
2023-04-24 20:14:32| cri

Zaidi ya viwanda vidogo vidogo 500 vya Wachina vimewekezwa Tanzania ambavyo vimewezesha Watanzania wengi kupata ajira.

Hayo yamebainika wakati Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Pendo Malangwa alipofungua mashindano ya awali ya Siku ya Lugha ya Kichina Duniani yaliyoadhimishwa chuoni hapo.

Profesa Malangwa amesema asilimia kubwa ya Watanzania walioajiriwa katika viwanda hivyo ni wale wanaojua lugha ya Kichina kupitia elimu inayotewa na Taasisi ya Confucius iliyopo chuoni hapo.

Amesema kupitia viwanda hivyo Watanzania wanaojifunza lugha ya Kichina wanaweza kuajirika katika viwanda hivyo. Amesema Wachina wana mchango mkubwa katika kuunganisha nchi za Afrika na China kupitia taasisi yake ya Confucius ambayo kazi yake kubwa ni kufundisha lugha ya Kichina, utamaduni wake na michezo mbalimbali inayoendana na utamaduni wa Kichina.