Ethiopia yasifiwa kwa kusaidia kuwahamisha watu waliopo Sudan huku mapigano yakizidi kupamba moto
2023-04-25 23:20:38| cri

Serikali ya Marekani imeipongeza Ethiopia kwa kusaidia katika juhudi za kuhamisha watu, huku serikali za kigeni zikijitahidi kuwaokoa wanadiplomasia, wafanyakazi na raia wao waliokwama nchini Sudan.

Mataifa yenye nguvu duniani Marekani na Uingereza yamewasafirisha kwa ndege wanadiplomasia wao kutoka Khartoum, lakini baadhi ya nchi ambazo hazikuweza kuwasafirisha raia wao kwa ndege zimekuwa zikitumia njia nyingine, ikiwa ni pamoja na kusafiri kwa barabara kupitia mipaka ya Ethiopia na Djibouti. Watu hao wanaingia Ethiopia kupitia mpaka wa Galabat-Metema ambapo watasafiri hadi Addis Ababa wakisubiri kurejeshwa nchini kwao.

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia Balozi Meles Alem, Ethiopia inashirikiana na baadhi ya nchi kuwahamisha raia wao kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu. Bado haijabainika ni watu wangapi au ni mataifa gani ambayo yamehamishwa hadi Ethiopia hadi sasa.