Somalia imeadhimisha Siku ya Chanjo Duniani jumatatu wiki hii na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kuimarisha huduma ya afya ya msingi na utaratibu wa kawaida wa utoaji chanjo nchini humo, na kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma.
Wizara ya Afya ya Somalia kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), imesema imepata maendeleo makubwa mwaka jana katika kuondoa pengo katika utoaji wa chanjo kwa kuongeza juhudi za kuboresha utaratibu wa kawaida wa chanjo nchini humo.
Waziri wa Afya nchini Somalia, Ali Haji ameyapongeza mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa kwa kufanya uratibu na wenza wa pande nyingi na kusaidia serikali ya Somalia kupata mafanikio katika kutoa chanjo muhimu.