Idadi kubwa ya watu wameathiriwa na ugumba ama utasa katika maisha yao, ambapo 17.5% ya idadi ya watu wazima ambao ni takriban 1 kati ya 6 duniani kote hupata tatizo la kutoweza kuzaa, na kuashiria kwamba kuna haja ya dharura ya kuongeza upatikanaji wa huduma ya uzazi ya bei nafuu na ya hali ya juu kwa wale wanaohitaji.
Makadirio mapya yanaonesha tofauti ndogo katika kuenea kwa utasa kati ya kanda. Viwango hivi vinalinganishwa kwa nchi zenye kipato cha juu, cha kati na cha chini, na kuonesha kuwa hii ni changamoto kubwa ya kiafya duniani kote. Kiwango cha tatizo hili ni 17.8% katika nchi za kipato cha juu na 16.5% katika nchi za kipato cha chini na cha kati.
Utasa ama ugumba ni ugonjwa wa mfumo wa uzazi wa mwanamume au mwanamke, unaofafanuliwa kwa kushindwa kupata ujauzito baada ya miezi 12 au zaidi ya kujamiiana mara kwa mara bila kinga. Inaweza kusababisha kadhia kubwa, unyanyapaa, na ugumu wa kifedha, na kuathiri ustawi wa kiakili na kisaikolojia wa watu. Hivyo leo katika kipindi cha ukumbi wa wanawake tutaangalia kwa ujumla tatizo hili kwa wanawake na njia za kutibu ama kukabiliana nalo.