WHO yaonya kuhusu hatari ya kibaolojia nchini Sudan huku kusitishwa kwa mapigano kukiruhusu wengi kukimbia
2023-04-26 19:04:33| cri

Mapigano nchini Sudan yalitulia usiku kucha wa siku ya Jumanne baada ya jeshi na kikosi pinzani cha wanamgambo kukubaliana kusitisha mapambano kwa siku tatu na kuruhusu Wasudan zaidi kukimbia na mataifa ya kigeni kuwaondoa raia wao.

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema kuna "hatari kubwa ya kibaolojia" katika mji mkuu Khartoum baada ya moja ya pande zinazopigana kushikilia maabara ya kitaifa yenye vimelea vya magonjwa ya surua na kipindupindu na kuwafukuza mafundi.

Vita vilivyozuka kati ya jeshi na Vikosi Vya Msaada wa Haraka (RSF) Aprili 15 vimegeuza maeneo ya makazi kuwa medani ya vita, na kuua watu wasiopungua 459, kujeruhi zaidi ya 4,000, na kukata maji, umeme na chakula katika taifa hilo ambalo tayari linategemea msaada.

Nchi za kigeni zimewasafirisha kwa ndege wafanyakazi wa ubalozi kutoka Khartoum, baada ya mashambulizi kadhaa dhidi ya wanadiplomasia, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa mwambata wa Misri aliyepigwa risasi akielekea kazini. Nchi nyingine pia zinachukua raia wao.