Asilimia 94 wana hatari kuambukizwa malaria Tanzania
2023-04-26 18:02:43| cri

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema licha ya kupungua kwa vifo na maambukizi ya malaria nchini Tanzania, bado asilimia 94 ya Watanzania wako hatarini kupata ugonjwa huo.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri Ummy amesema maambukizi ya malaria yamepungua kutoka asilimia 18.4 mwaka 2015 hadi asilimia 8.1 mwaka 2022, lakini bado wanashuhudia vifo na Watanzania wakipata ugonjwa wa malaria. Amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wanatekeleza mpango wa miaka mitano wa kutokomeza malaria, ambapo wamejikita katika mambo manne, ambayo ni udhibiti wa mbu wanaoeneza malaria, uchunguzi, tiba, kinga na ufuatiliaji na tathmini ya mwendo wa malaria.

Wakati huohuo Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amemteua mwimbaji wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul Diamond Platnumz na mjasiriamali Zuwena Mohamed ‘Shilole’ kuwa Wajumbe wa Baraza la Taifa la Kutokomeza Malaria.