Mratibu wa Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Adam Abdelmoula amesema, jumla ya dola za kimarekani milioni 112 zimetolewa kwenye Mfuko wa Kibinadamu wa Somalia ili kukabiliana na ukame mkali nchini humo kwa mwaka jana.
Katika ripoti yake ya mwaka, Abdelmoula amesema, idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi nchini Somalia imeongezeka na kufikia milioni 7.8 mwaka jana, kutoka watu milioni 5.9 mwaka 2021. Amesema Somalia bado inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu kutokana na ukame unaoendelea, mapigano, bei kubwa ya chakula na maji, na wakimbizi wa ndani.
Amewapongeza wafadhili kwa kuongeza michango yao kutoka dola za kimarekani milioni 58.7 mwaka 2021 hadi dola milioni 67 mwaka jana.