Waziri Mchengerwa atoa maagizo wanyama waliovamia makazi ya watu waondolewe
2023-04-28 23:26:57| cri

Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa ameziagiza taasisi za serikali hifadhi za wanyamapori na misitu kuwatumia askari 231 waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi Kituo cha Mlele, kuwatoa wanyama wakali wanaovamia maeneo ya wananchi na kusababisha taharuki kubwa.

Waziri Mchengerwa ametoa agizo hilo Aprili 26, 2023 katika hafla ya ufungaji mafunzo hayo iliyofanyika katika kituo cha mafunzo Mlele kwa askari wa Hifadhi ya Ngorongoro na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

Amesema wanyama hao wakali na waharibifu wa mali za wananchi wanasababisha malalamiko, masononeko, majeraha na wakati mwingine vifo miongoni mwao hususani wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi.