Wakurugenzi wa afya kutoka nchi za Afrika wamesema, ongezeko la mzigo wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza barani Afrika unaweza kudhibitiwa mara bara hilo litakapotoa kipaumbele katika uwekezaji wa vifaa vya kisasa vya ugunduzi.
Naibu rais wa kampuni ya kimataifa ya madawa ya Roche Diagnostic Afrika, Allan Pamba amesema, maboresho katika vifaa vya vipimo vya malaria, VVU na UKIMWI, homa ya manjano, magonjwa ya moyo, kisukari na saratani yataboresha tiba zake na huduma huku yakipunguza idadi ya vifo kwa wagonjwa.
Kaimu mkuu wa kampuni hiyo katika Nchi zinazozungumza Kiingereza kanda ya Afrika Magharibi, Taofik Oloruko-Oba, amesisitiza kuwa, mtazamo mpya kwa ajili ya miundombinu inayofaa ya utambuzi katika taasisi za afya barani Afrika unatakiwa ili kukabiliana na mzigo mkubwa wa magonjwa unaohusishwa na mtindo mbaya wa maisha.
Naye Mkurugenzi wa Mageuzi ya Mkakati na Huduma za Afya wa kampuni hiyo barani Afrika, Jonathan Ketel amesema, nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza katika vifaa vya utambuzi ili kuboresha vipimo vya magonjwa kama sehemu ya ajenda ya kimataifa ya afya kwa wote.