Viongozi wa kikanda kutoka nchi zilizopeleka askari wake katika tume ya ulinzi wa amani nchini Somali, wamekutana nchini Uganda jana alhamis, kujadili mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa na mipango ya kuanza kuondoa askari hao nchini Somalia.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter, rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema mkutano huo umehudhuriwa na rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh, rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, rais wa Kenya William Ruto, rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, na Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Demeke Mekonnen.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limependekeza kuondolewa kwa vikosi hivyo nchini Somalia ili kuruhusu jeshi la nchi hiyo kutekeleza operesheni zote za ulinzi wa amani.