Ubalozi wa Afrika Kusini nchini China waadhimisha siku ya Uhuru
2023-04-28 18:24:56| cri

Ubalozi wa Afrika Kusini nchini China jana uliadhimisha siku ya uhuru ambayo inafanyika kila ifikapo tarehe 27 Aprili.

Kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika katika hoteli ya Kempiski hapa Beijing balozi wa Afrika Kusini nchini China Siyabonga Cwele alisema Afrika Kusini imepata maendeleo makubwa katika kurejesha utu na kuboresha maisha ya watu wake tangu mwaka 1994 nchi hiyo ifanikiwe kuwa ya kidemokrasia. Amebainisha kuwa katika kipindi chote hicho wameondokana na vitendo vya ubaguzi wa rangi na kujiunga na familia ya kimataifa pamoja na uchumi wa dunia. 

 “Tunatoa heko kwa Harakati za kimataifa za Kupinga ubaguzi wa rangi ambazo zilipeleka mapambano yetu kuingia mitaani na vijijini duniani. Hapa China, mwaka 1953 Walter Sisulu, Katibu Mkuu wa African National Congress alikutana na Mwenyekiti Mao ambaye mara moja alitoa msaada usioyumba kwa ajili ya uhuru wetu.” alisema balozi Cwele kwenye hotuba yake.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya miaka 25 tangu Afrika Kusini na China zianzishe uhusiano wa kibalozi ambayo yaliambatana na sherehe hizi za uhuru, balozi Cwele amesema chini ya muongozo wa rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na mwenzake wa China Xi Jinping, maingiliano ya mara kwa mara kati ya nchi hizi mbili yamefanyika katika ngazi mbalimbali rasmi, yakijumuisha ziara za kiserikali na mashirikiano ya hali ya juu katika ngazi ya wizara, mabunge ya pande mbili, biashara na kuunganisha watu wa nchi hizi mbili.