Maafisa wa Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali wamesema vifo vinavyotokana na njaa vinaongezeka barani Afrika kwa sababu ya ukame unaochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa na migogoro.
Wakizungumza kwenye mkutano wa pamoja na wanahabari mjini Paris maafisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na NGOs Care na Oxfam walisema kuna vifo vya njaa kila baada ya sekunde 36 kwa wastani nchini Ethiopia, Kenya na Somalia. Wameongeza kuwa takriban watu milioni 20 katika eneo la Sahel wanaishi kwenye uhaba wa chakula.
UNICEF ilisema nchini Burkina Faso, nchi iliyovurugwa na waasi wa jihadi, idadi ya watoto waliofariki kati ya Januari na Septemba 2022 ni mara tatu zaidi kuliko ile ya kipindi kama hicho mwaka wa nyuma yake. Idadi ya watoto waliotibiwa kwa utapiamlo mbaya iliongezeka kwa asilimia 50.
Louis-Nicolas Janeaux wa Oxfam Ufaransa, alisema nchini Niger ukame wa mara kwa mara na mafuriko mabaya pamoja na migogoro inayoendelea ilisababisha kupungua kwa karibu asilimia 40 ya uzalishaji wa nafaka huku uvunaji ukizidi kuwa mgumu.
Kwa upande wake msemaji wa UNICEF Lucile Grosjean alisema watoto wapatao 430,000 nchini Niger wanakabiliwa na utapiamlo mbaya.
Mwaka huu, idadi ya wanawake wajawazito au wanaonyonyesha walio na utapiamlo inakadiriwa kuongezeka hadi 154,000 kutoka 64,000 ya mwaka 2022.