Jeshi la polisi la Tanzania limesema watoto 37 wamefariki dunia kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika mikoa tisa nchini Tanzania kuanzia Januari na Aprili 28.
Msemaji wa jeshi hilo Bw. David Misime, amesema katika taarifa yake kwamba baadhi ya watoto hao walisombwa na mafuriko, na wengine kuzama kwenye visima na madimbwi yaliyofurika.
Amesema watoto hao walifariki katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Kigoma, Mwanza, Pwani, Katavi, Morogoro na Rukwa, na pia amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanazuiliwa kutoka nje ya nyumba wakati wa mvua.
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania imekuwa ikitoa tahadhari kila siku kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini ambazo huenda zikasababisha mafuriko na madhara makubwa.