Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kiarabu wajadili msukosuko wa Syria
2023-05-02 09:00:02| CRI

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jordan, Saudi Arabia, Iraq, Misri na Syria jana walikutana mjini Amman, Jordan ili kutafuta suluhisho la kisiasa la msukosuko wa kibinadamu, kiusalama na kisiasa nchini Syria.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Jordan, imesema mawaziri hao wamesema suluhisho hilo linatakiwa kuchangia katika kurejea kwa hiari na salama kwa wakimbizi, kuondoka kwa majeshi yasiyo halali na kurejeshwa kwa usalama na utulivu nchini Syria. Pia wamekubaliana kuimarisha ushirikiano na jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa katika kuhimiza utekelezaji wa miradi mapema, ikiwa ni pamoja na kutoa miundombinu iliyoboreshwa na maisha yenye heshima kwa wakimbizi wanaotaka kurejea.

Mawaziri hao pia wamekubaliana kuiunga mkono Syria katika kulinda mamlaka yake halali ya ardhi kwa kutekeleza sheria, kutokomeza makundi ya kigaidi na kuzuia uingiliaji wa nje kwenye mambo ya ndani ya nchi hiyo.