Mratibu wa misaada wa UM ajitahidi kuendeleza operesheni za kibinadamu nchini Sudan
2023-05-02 08:44:39| CRI

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema, mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja huo Bw. Martin Griffiths na wadau wengine wanafanya kila juhudi kurejesha mwitikio wa kibinadamu kwa msukosuko unaoendelea nchini Sudan.

Msemaji huyo amesema Bw. Griffiths ametumwa kutafuta njia za kufikisha misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu ambao maisha yao yamevurugika kutokana na mapambano yanayoendelea nchini Sudan.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, Bw. Griffiths sasa yuko Nairobi ambako amekutana na Rais William Ruto wa Kenya, waziri wa mambo ya nje wa Canada Melenie Joly ambaye yuko ziarani nchini humo na wengine, ili kujadili hali tete nchini Sudan. Kwa hatua ijayo, Bw. Griffiths atajitahidi kuratibu na kuongeza misaada ya kibinadamu nchini Sudan.