Mjumbe wa China ataka Umoja wa Mataifa uimarishe utendaji kamili wa bajeti ya ulinzi wa amani
2023-05-02 08:41:11| CRI

Naibu mjumbe wa China kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Dai Bing ametoa wito kwa Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kuimarisha utendaji kamili wa bajeti ya ulinzi wa amani, ili kuongeza ufanisi wa shughuli za ulinzi wa amani.

Akiongea kwenye kikao cha kamati ya tano cha mkutano wa 77 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Balozi Dai amesema ikiwa ni bajeti kubwa zaidi ya Umoja wa Mataifa yenye thamani ya mabilioni ya dola, China daima inaunga mkono juhudi za kamati ya tano kupitia upya bajeti hiyo chini ya kanuni ya msingi wa sayansi na busara, na kutoa raslimali muhimu kwa ajili ya operesheni za kulinda amani.

Amesema China inaunga mkono bodi ya wakaguzi katika kutekeleza kikamilifu jukumu lake kama chombo cha ukaguzi ili kutoa mapendekezo muhimu kuhusu kuboresha usimamizi wa bajeti. Pia amesema China inaunga mkono Umoja wa Mataifa kuzilipa kwa wakati nchi zinazochangia wanajeshi na polisi.