Wanasayansi wa Afrika wahimiza kujiandaa kikamilifu ili kudhibiti magonjwa ya kuambukiza
2023-05-02 08:41:46| CRI

Wanasayansi wa Afrika wamezitaka nchi za Afrika katika eneo la kusini mwa Sahara, kuimarisha ufuatiliaji, na kuwekeza katika chanjo mpya, upimaji na matibabu ili kupunguza tishio linaloongezeka la magonjwa ya kuambukiza.

Akiongea mjini Nairobi kwenye kongamano la Wiki ya Usimamizi ya Ibrahim 2023 lililomalizika hivi karibuni, mkurugenzi mtendaji wa mfuko wa Sayansi wa Afrika Bw. Tom Kariuki, amesisitiza kuwa kuimarisha utayari ni muhimu katika kuepusha changamoto dhidi ya mifumo ya afya ya umma barani Afrika kama magonjwa ya milipuko yatatokea.

Amesema Afrika inaendelea kukabiliwa na mzigo unaoongezeka wa magonjwa ya kuambukiza, unaochochewa na mabadiliko ya tabia nchi, kuvurugika kwa mifumo ya ikolojia na uchafuzi wa mazingira. Ameongeza kuwa suluhisho lipo katika kuongeza utengenezaji wa bidhaa za afya kama vile chanjo, dawa za kupambana na bakteria na kutoa elimu zaidi kwa umma.