Israel yafanya mashambulizi dhidi ya Gaza baada ya kushambuliwa kwa maroketi
2023-05-03 08:51:57| CRI

Israel imefanya mashambulizi ya anga katika maeneo ambayo ni ya makundi ya wanamgambo wa Palestina yanayoongozwa na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Maofisa wa usalama wa Palestina huko Gaza wamesema ndege zisizo na rubani za Israel na ndege za kivita zilizunguka katika eneo la ukanda wa Gaza, na kisha milipuko kadhaa ilisikika.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema katika taarifa kuwa vikosi vya anga vya Israel vimefanya mashambulizi hayo ili kujibu mashambulizi ya maroketi yaliyofanywa hapo awali kutoka eneo la kusini mwa Israel. Jana makundi ya wanamgambo wa Kipalestina yalidai kuwajibika na urushaji wa maroketi 37 na makombora kusini mwa Israel.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema katika taarifa yake kuwa maofisa waandamizi wa usalama wa nchi hiyo walikuwa na mkutano maalum wa kutathmini hali, ambapo hatua za kijeshi zilijadiliwa.