Klabu ya PSG yaimarisha usalama baada ya maandamano yaliyowalenga Neymar na Messi
2023-05-05 19:11:58| cri

Klabu ya Paris Saint-Germain imeamuru kuwepo na usalama wa ziada katika uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo na katika nyumba za Lionel Messi na Neymar baada ya maandamano ya mashabiki waliokasirishwa na matokeo ya hivi karibuni ya viongozi hao wa Ligue 1.

Mamia ya wafuasi wa PSG walikusanyika nje ya makao makuu ya klabu Jumatano jioni ambapo waliwasha moshi na kuimba nyimbo za chuki kuhusu nyota ambao hawakufanya vizuri Messi, Neymar na kiungo wa Italia Marco Verratti. Baadhi yao, wakiwa wamevalia nguo nyeusi, walikwenda hadi nyumbani kwa Neymar katika kitongoji cha matajiri magharibi mwa Paris ambako waliimba "Neymar, potea".

Kwa upande wake Paris Saint-Germain ilitoa taarifa Jumatano jioni ikilaani kwa nguvu zote vitendo hivyo visivyokubalika na vya matusi vya kikundi kidogo cha watu binafsi, na kusema hata wawe na maoni tofauti hakuna kinachohalalisha tabia kama hiyo.

Neymar, ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha katika klabu ya PSG na yuko nje hadi mwisho wa msimu huu, alijibu kwa kuandika kwenye Instagram: "Usiwaruhusu watu wakuweke kwenye dhoruba yao. Waweke kwenye amani yako."