Mkurugenzi wa IMF apongeza mpango wa kufufua uchumi wa Kenya
2023-05-05 08:56:16| CRI

Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF Bibi Kristalina Georgieva ambaye yuko ziarani nchini Kenya, ameeleza imani yake kuhusu mpango wa kufufua uchumi wa Kenya.

Akiongea kwenye mkutano wake na Rais Willian Ruto, Bibi Georgieva amepongeza hatua za kifedha zinazochukuliwa na Kenya na kusema hatua hizo ni mwelekeo sahihi.

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Kenya inasema Bibi Georgieva amepongeza msukumo wa uwekezaji, hatua makini za kifedha na uwazi kwenye utawala.

Pongezi za Bibi Georgieva zimekuja wakati Kenya imeanza mpango wa kukusanya fedha kwenye masoko ya kimataifa kupitia dhamana za kifedha, ili kupunguza nakisi ya bajeti ya dola za kimarekani bilioni 2.