Tarehe 23 May ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Fistula. Historia ya Siku hii ilianza wakati Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) lilipozindua kampeni ya “Kumaliza Fistula” mwaka 2003. Mwaka 2013, miaka 10 baadaye, Umoja wa Mataifa ulianza kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Fistula ya Uzazi, na kuifanya kuwa kampeni ya kila mwaka.
Fistula ya uzazi ni jeraha linalohusana na uzazi ambalo linawaathiri sana wanawake, hususan wale walio katika nchi masikini. Ugonjwa wa Fistula ya uzazi huwapata wanawake wakati wa kujifungua hasa wale wanaojifungua wakiwa na umri mdogo pamoja na kukosa msaada stahiki wakati wa kujifungua, ambapo viungo kama kibovu cha mkojo na njia ya haja kubwa hujeruhiwa na kusababisha mwanamke ashindwe kujizuia haja ndogo au kubwa. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka Afrika na Asia wanaishi na ugonjwa huu, bila kupatiwa matibabu yoyote. Katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake leo hii, tunaangazia zaidi ugonjwa huu na athari zake kwa wanawake.