Syria yarejea Jumuiya ya Nchi za Kiarabu baada ya kutokuwepo kwa miaka 12
2023-05-08 09:53:44| CRI

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wameamua kuirejeshea uanachama wake Syria katika jumuiya hiyo baada ya kusimamishwa kwa miaka 12. Uamuzi huo umefikiwa kwenye mkutano wa dharura uliofanyika mjini Cairo, Misri jana Jumapili.

Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imesema kuwa mkutano wa baraza la AL wa ngazi ya mawaziri uliamua kurejesha tena ushiriki wa wajumbe wa serikali ya Syria katika mikutano ya baraza la AL na mashirika na vyombo vyake vyote kuanzia tarehe 7 Mei, mwaka 2023.

Mawaziri hao pia walikubaliana juu ya umuhimu wa kuongeza juhudi za kuisaidia Syria kutoka katika mgogoro wake. Taarifa hiyo imesema kuwa wamerejesha upya dhamira yao ya kulinda mamlaka ya Syria, ukamilifu wa ardhi, utulivu, na mafungamano ya kikanda kwa kuzingatia mkataba wa AL na kanuni zake.

Mawaziri hao wa mambo ya nje pia walikubaliana kuunda kamati inayojumuisha Jordan, Saudi Arabia, Iraq, Lebanon, Misri, na Katibu Mkuu wa AL kuendelea na mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Syria ili kufikia suluhu ya kina kwenye mgogoro wa Syria.