Watu 23 wamefariki na wengine 16 kujeruhiwa baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha maporomoko ya udongo katika vijiji kadhaa katika wilaya za Kisoro, Rubanda, Rukiga, na Ntoroko.
Kufuatia janga hilo, rais wa Uganda Yoweri Museveni ameomboleza vifo vya watu hao magharibi mwa nchi hiyo wiki iliyopita, na kusema atatoa msaada wa kifedha kwa familia za marehemu hao.
Katika taarifa yake, rais Museveni ametoa maelekezo kwa Mdhibiti Fedha wa Ikulu kutoa Shilingi za Uganda milioni 5 kwa kila familia ya marehemu, na shilingi milioni moja kwa watu waliojeruhiwa katika wilaya tatu za mkoa wa Kigezi na wilaya ya Ntoroko.
Mwezi uliopita, Uganda ilitoa tahadhari ya kutokea kwa majanga, na kuonya kuwa maeneo kadhaa ya nchi hiyo yatakumbwa na mafuriko, maporormoko ya udongo, mvua za mawe na radi wakati msimu wa kwanza wa mvua ukianza.