Hivi karibuni Benki Kuu ya Marekani iliongeza kiwango cha riba kwa mara ya kumi ndani ya miezi 14 iliyopita, hatua ambayo imelaumiwa tena ndani na nje ya nchi hiyo. Kuendelea kuongeza kiwango cha riba sio tu kunaifanya Marekani kukaribia kwenye msukosuko wa kiuchumi, lakini pia kunasababisha nchi nyingi zaidi kujiunga na wimbi la kimataifa la kuacha kutumia dola ya Marekani.
Kutokana na nguvu kubwa isiyo na kifani ya dola ya kimarekani, serikali ya Marekani kuongeza kiwango cha riba kwa raundi kadhaa kumesababisha kuendelea kupanda kwa thamani ya dola, kushuka kwa thamani ya sarafu za nchi nyingine na kisha kupanda kwa gharama za maisha. Kama eneo lililoathiriwa zaidi, wastani wa mfumuko wa bei barani Afrika ulifikia 13.5% mwaka 2022, kiwango cha juu zaidi katika muongo mmoja. Kwa hiyo nchi nyingi zaidi zinatafuta njia za kujiokoa, ikiwa ni pamoja na kuepuka kutumia dola katika biashara za pande mbili na za kimataifa, na kupanga kuanzisha mifumo yao ya kibiashara. Hivi karibuni serikali ya Kenya ilitangaza kwamba itaacha dola na kutumia shilingi ya Kenya katika kuagiza mafuta kutoka nje. Hii sio tu itasaidia Kenya kupunguza hatari zinazohusiana na fedha za kigeni ikiwemo athari ya kubadilika kwa thamani ya dola kwa uchumi wa nchi hiyo, lakini pia itakuza zaidi mchakato wa mafungamano wa kiuchumi barani Afrika.
Wimbi la "kuacha kutumia dola" pia ni matokeo ya serikali ya Marekani kutumia dola kama silaha ya kukandamiza nchi nyingine. Mtaalamu wa siasa za kijiografia wa Ufaransa Bw. Renaud Girard, hivi karibuni aliandika makala kwenye gazeti la Le Figaro akitoa mfano wa benki ya BNP Paribas, akisema mwaka 2014 benki hiyo ilitozwa faini ya dola bilioni 9 na Marekani kwa madai kuwa ilifanya biashara na Iran, Sudan na Cuba. Kwa kutoza faini, serikali ya Marekani inazuia nchi nyingine kufanya biashara na nchi zilizowekewa vikwazo na Marekani kutumia dola. Baada ya kuibuka kwa mgogoro kati ya Russia na Ukraine, uchumi wa Russia uliwekewa vikwazo vikali na Marekani, na nchi zimefahamu zaidi kwamba hifadhi zao za dola ziko hatarini kuporwa kihalali au kinyume cha sheria wakati wowote, na kuzidi kuwa na makubaliano kuhusu kuacha kutegemea dola. Ni wazi kuwa kadiri dola inavyotumika kama silaha, ndivyo kasi ya kutaka kuacha matumizi ya dola inavyoongezeka.
Siku hizi nchi mbalimbali duniani zinaimarisha uwepo wa sarafu mseto na kuongeza hadhi ya sarafu zao kwenye biashara ya kimataifa. Mbali na sarafu za jadi zenye nguvu kama vile Euro na Yen ya Japan, sarafu za nchi zinazoibukia sokoni ikiwemo RMB pia zinaimarika taratibu. Mwishoni mwa mwezi Machi, kampuni ya nishati ya Total ya Ufaransa na CNOOC ya China, zilisaini biashara ya kwanza ya gesi asilia iliyoyeyushwa iliyofungwa kwa RMB, na kuifanya Ufaransa kuwa nchi ya kwanza ya Ulaya kukubali kulipa kwa RMB badala ya dola au Euro. Habari zinasema zaidi ya nchi 30, ikiwa ni pamoja na Brazil, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Russia na Iran, zinatumia RMB katika biashara na uwekezaji.
Zaidi ya miaka 50 iliyopita, aliyekuwa waziri wa fedha wa Marekani John Connally, alisema "Dola ni sarafu yetu, lakini ni shida yenu." Matumizi mabaya ya nguvu ya dola yamepunguza imani za nchi nyingine kwa Marekani na dola. Kwa mujibu wa takwimu ya Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, uwiano wa hifadhi ya dola duniani umeshuka kutoka zaidi ya 70% mwaka 2000 hadi karibu 56% kwa sasa. Ingawa mchakato wa sasa si wa haraka sana, mwelekeo wa kimataifa wa "kuacha kutumia dola" unaokuzwa na serikali ya Marekani hauwezi kuzuiwa, na hatimaye kuwa shida ya Marekani yenyewe.