Idadi ya watu waliouawa kutokana na imani za kidini nchini Kenya yafikia 133
2023-05-10 09:17:42| CRI

Polisi nchini Kenya imefukua miili 21 zaidi kutoka kwenye kaburi moja katika mji wa pwani wa Malindi nchini humo.

Polisi wamesema, mpaka sasa, miili 133 imefukuliwa tangu kugunduliwa kutoka kwa makaburi ya watu wengi katika sehemu ya ardhi iliyoko kwenye msitu wa Shakahola mwishoni mwa mwezi April.

Wachunguzi wa polisi walioendelea na msako wa makaburi mengine ya watu wengi jana jumanne, wamesema miili mingi ni ya watoto walioambiwa na mtu anayejiita mchungaji Paul Nthenge kufunga mpaka kufa ili kukutana na Yesu.

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki amesema, mchakato wa ufukuaji wa makaburi hayo ulifanyika kwa umakini ili kulinda hadhi na faragha za familia za marehemu. Ameongeza kuwa, juhudi za uokoaji zinaendelea, na mpaka sasa, watu 65 wameokolewa kutoka kwenye msitu huo, wakiwemo wawili ambao waliokolewa jana asubuhi na wachunguzi wa polisi.