Sudan Kusini na Misri zatoa wito wa juhudi za pamoja kwenye kukabiliana na mgogoro wa kibinadamu katika mpaka wa Sudan
2023-05-10 09:09:08| CRI

Sudan Kusini na Misri zimetoa wito wa kufanya juhudi za pamoja kati ya nchi jirani na Sudan na jumuiya ya kimataifa ili kukabiliana na mgogoro wa kibinadamu unaotokana na vurugu zinazoendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Akizungumza na wanahabari mjini Juba akiwa na mwenzake wa Misri, Sameh Hassan Shoukry, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini, Deng Dau Deng amesema, mgogoro wa kibinadamu unaoendelea kutokana na mapigano nchini Sudan tayari umehatarisha rasilimali haba kwa nchi jirani kujibu kwa ufanisi wimbi la watu wanaokimbia mapigano katika maeneo ya mpakani.

Naye Waziri Shoukry amesisitiza haja ya uratibu wa karibu kati ya Misri na Sudan Kusini katika kutatua suala la Sudan. Amesema nchi hizo mbili zitashirikiana kwa karibu kuzitaka pande zinazopigana nchini Sudan kufikia makubaliano ya kusimamisha mapigano na kurejea katika majadiliano ya kisiasa ili kutatua tofauti zao.