Mtanzania wa kwanza apata cheti cha asili ya bidhaa cha kufanya biashara kwenye eneo la biashara huria la Afrika (AfCFTA)
2023-05-11 21:40:16| cri

Kaimu Makamu Mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo cha Tanzania (TCCIA), Bw. Vicent Minja, amesema mtanzania wa kwanza alipokea cheti cha asili jana kufanya biashara katika Eneo Huria la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).

Akikabidhi cheti hicho jana, Bw. Minja amesema cheti hicho kitamruhusu mfanyabiashara huyo kupata punguzo la ushuru wa forodha kutoka asilimia 35 hadi 12. Amesema hatua hiyo inatokana na juhudi za TCCIA kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu faida za kusafirisha bidhaa kwa kutumia vyeti vya asili ya bidhaa chini ya makubaliano ya Eneo Huria la Biashara ya Bara la Afrika.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Bw. Fortunatus Mhambe, amesema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakipuuza vyeti vya asili ya bidhaa katika shughuli zao za biashara bila kujua kuwa vyeti hivyo vitawarahisishia shughuli zao kwa kuwasaidia kupata masoko zaidi.

Amesema wakati Afrika imekuwa ikijitahidi kushinda changamoto nyingi za kiuchumi, hii ni fursa moja ya kusonga mbele, na kuwataka wamiliki wa biashara wa ndani kutumia fursa hii kupunguza vikwazo vya biashara.