Tanzania, Uganda zakubaliana kutatua vikwazo vya biashara
2023-05-11 21:41:19| cri

Serikali za Tanzania na Uganda zimekubaliana kushirikiana katika kuondoa vikwazo vya biashara ili kurahisisha shughuli hizo na kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo.

Makubaliano hayo yamefikiwa jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano wa Majadiliano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk Stergomena Tax, na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Bibi Rebecca Kadaga.

Bibi Kadaga amesema kazi ya pamoja itafanyika ili kuhakikisha vikwazo vilivyopo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha vinaondolewa. Hata hivyo, mkutano huo umewawezesha kukamilisha baadhi ya mambo yaliyokuwa mezani na kujipa muda hadi mwishoni mwa Julai 2023 kukamilisha machache yaliyobaki.

Dk. Tax ameongeza kuwa mbali na makubaliano hayo, nchi hizo pia zimekubaliana kujenga Kituo cha Uokoaji jijini Mwanza kitakachoshughulikia maafa yatakayotokea katika Ziwa Victoria. Kukamilika kwa kituo hicho kutarahisisha shughuli za uokoaji iwapo itatokea ajali yoyote katika Ziwa Victoria.