Waziri asema Afrika Kusini imenufaika na uanachama wa BRICS
2023-05-11 10:06:52| CRI

Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini Naledi Pandor amesema, nchi hiyo imenufaika na kuwa mwanachama wa kundi la BRICS, ikishuhudia kuongezeka kwa biashara na washirika na ufadhili wa kushughulikia baadhi ya changamoto za ndani.

Pandor amesema hayo jana Jumatano bungeni alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2023. Amesema ushirikiano wa nchi za BRICS umeleta manufaa yanayoonekana kwa Afrika Kusini katika sekta mbalimbali. Amesema thamani ya jumla ya biashara na nchi nyingine za BRICS imeongezeka kutoka randi bilioni 487 mwaka 2017 hadi bilioni 702 mwaka 2021. Pia nchi hiyo imepokea ufadhili wa zaidi ya dola bilioni 5 kutoka kwa Benki Mpya ya Maendeleo kwa ajili ya miradi muhimu ya miundombinu katika nishati mbadala, maji na sekta nyingine.

Amesema, nchi nyingi zimeonyesha nia ya kujiunga na BRICS, na lengo la Afrika Kusini kwa mwaka huu ni kuhakikisha kuwa BRICS inaimarika zaidi, na kuandaa mkutano wa kilele wenye mafanikio utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu.