Pande zinazopigana nchini Sudan zasaini makubaliano ya kuzuia kuwadhuru raia
2023-05-12 10:15:04| CRI

Shirika la Habari la Saudi Arabia, Al Arabiya limesema, wawakilishi wa jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) wamesaini makubaliano ya awali katika mji wa Jeddah yanayolenga kuepuka kuwadhuru raia.

Wawakilishi wa pande hizo zinazopigana wamesisitiza kuwa maslahi ya watu wa Sudan ni kipaumbele, na kukubali kuruhusu raia wote kuondoka katika maeneo yaliyozingirwa.

Makubaliano hayo yalithibitisha mamlaka na umoja wa Sudan na kukaribisha juhudi za upatanishi za nchi nyingine, na kutoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi yote ambayo yatawadhuru raia.

Wawakilishi wa pande hizo mbili walianza mazungumzo Jumamosi huko Jeddah kuhusu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano ili kuwezesha msaada wa dharura wa kibinadamu kuwafikia wahitaji katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita.