Mkutano wa kutangaza Maonyesho ya tatu ya Biashara na Uchumi kati ya China na Afrika umefanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, jana alhamis, na kukutanisha watu kadhaa wakiwemo maofisa wa ngazi ya juu, wanadiplomasia, wafanyabiashara, na ujumbe wa ngazi ya juu kutoka mji wa Yiyang, mkoani Hunan, nchini China.
Naibu Kamishna wa Kitengo cha Uwezeshaji wa Biashara katika Mamlaka ya Mapato ya Kenya, Teresa Wanjagua amesema, Kenya itafaidika sana na maonyesho hayo kutokana na nafasi yake kama kitovu cha ugavi na biashara katika kanda ya Afrika Mashariki.
Ofisa wa ngazi ya juu wa Ubalozi wa China nchini Kenya, Zhang Yijun amesema, maonyesho ya tatu ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika yaliyopangwa kuanza Juni 29 hadi Julai 2 mwaka huu mjini Changsha, Hunan, nchini China, yanatoa fursa kwa Kenya kutangaza bidhaa zake za kilimo katika soko kubwa la China.