Serikali ya China imetoa tani karibu 2,400 za mchele kwa serikali ya Sudan Kusini ili kuisaidia kukabiliana na mgogoro wa kibinadamu unaotokana na mapigano katika nchi jirani ya Sudan.
Waziri wa Masuala ya Kibinadamu na Udhibiti wa Majanga wa Sudan Kusini, Albino Akol Atak amesema, msaada huo umewasili katika wakati muhimu ambapo wanajitahidi kukusanya rasilimali ili kukabiliana na idadi kubwa ya watu wanaoingia nchini humo kukimbia mapigano katika eneo la mpaka na Sudan.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Sudan Kusini Ma Qiang amesema, sehemu ya msaada huo wa chakula uliotolewa na serikali ya China itasambazwa kwa wakimbizi wa Sudan Kusini wanaorejea makwao.
Amesema Sudan Kusini ni moja ya nchi zilizo hatarini zaidi duniani zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, na kuongeza kuwa China imekuwa ikitoa msaada wa chakula kwa Sudan Kusini kwa miaka mingi, na kusaidia watu zaidi ya milioni moja.