Ulaya inaihitaji China kwa ajili ya soko lake kubwa pamoja na amani
2023-05-15 16:20:19| cri

Kwa muda sasa, uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya umekuwa kwenye mwelekeo wa kudorora, lakini mkwamo katika uhusiano huo ulianza kubadilika baada ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Baraza ka Ulaya Charles Michel kufanya ziara nchini China mwishoni mwa mwaka jana.

Katika mwezi huu, viongozi wa nchi za Ulaya wamekuwa wakifanya ziara nchini China mmoja baada ya mwingine, akiwemo Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sanchez, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na rais wa Kamati ya Ulaya, Ursula von der Leyen, na pia Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Ulaya kuhusu Masuala ya Kigeni na Sera za Usalama, Joseph Borrell, pia anatarajiwa kufanya ziara nchini China hivi karibuni.

Ni kwa nini basi viongozi hawa wa Ulaya wanaiangalia China kwa jicho la tatu?

Kwanza, kufufuka kwa uchumi wa Ulaya kunahitaji sana soko kubwa la China. Miaka michache iliyopita, serikali ya Marekani iliongoza katika utekelezaji wa sera za kujilinda kiuchumi, hatua iliyoathiri sana utandawazi wa uchumi duniani. Baadaye, janga la virusi vya Corona (COVID-19) lilisababisha kwa kiasi kikubwa kushuka kwa uchumi wa dunia, na baada ya vita ya Russia na Ukraine kutokea, Umoja wa Ulaya uliweka vikwazo kadhaa kwa Russia, na hivyo kuchochea tatizo la nishati katika bara hilo.

Kutokana na mambo hayo, pamoja na mpango wa kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka Russia na kuharakisha mageuzi ya kijani, uchumi wa Ulaya umejikuta ukikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo kupanda kwa gharama ya maisha, ukosefu wa ajira, bei kubwa ya umeme, kuongezeka kwa deni la serikali, na kupungua kwa soko la nje. Haya mambo yote yamefanya uchumi wa Ulaya kudumaa, na hivyo kuathiri vibaya maisha ya watu, na kutishia mfumo wa muda mrefu wa ustawi. Kwa kuwa Ulaya imeendelea kuwa mwenzi muhimu wa uchumi na biashara wa China, kudumisha na kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi na China ni uamuzi muhimu kwa bara hilo ili kujikwamua kutoka kwenye mzozo wa kiuchumi.

Pili, Ulaya inahitaji kuimarisha ushirikiano na China ili kuendeleza mkakati wake wa kujitawala. Tangu kutokea kwa vita ya Russia na Ukraine, Ulaya imetumia rasilimali muhimu, hususan za kijeshi, kuiunga mkono Ukraine dhidi ya Russia, na matokeo yake, uhusiano wa bara hilo na NATO na Marekani umekuwa wa karibu zaidi katika maeneo ya ulinzi na siasa, lakini maendeleo ya maingiliano ya ulinzi wa ndani yara hilo yamesimama. Wakati huohuo, kuimarisha uhusiano wa ng’ambo ya bahari ya antlantiki na kutegemea zaidi Marekani kumeongeza shinikizo kwa Ulaya, na hii haiendani na maslahi yake. Sasa ili kuendeleza mkakati wake wa kujitwala na kulinda maslahi yake, Ulaya inahitaji kuimarisha uhusiano wake na China ili kuweza kuondokana na udhibiti wa Marekani.

Tatu, Ulaya inahitaji uungaji mkono wa China kusaidia kusuluhisha mgogoro wa Russia na Ukraine. Mgogoro huo ni tishio kubwa la usalama wa kikanda ambao Ulaya umekabiliwa nao tangu vita ya Bosnia na Kosovo katika miaka ya 1990. Vita hiyo inaharibu maslahi ya kimsingi ya bara la Ulaya, na kutokana na msimamo wa China katika mgogoro huo ambao haupendelei upande wowote, ni muhimu sana kwa Ulaya kushirikiana na China katika kusuluhisha mgogoro huo.

Nne, Umoja wa Ulaya unaihitaji China katika kutatua masuala ya utawala wa dunia. Umoja wa Ulaya una msimamo mkali katika eneo la uongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ukijaribu kuwa kiongozi wa kimataifa katika eneo hilo. China, kama mshiriki katika uongozi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ni mwenzi wa kutegemeka wa Ulaya. Zaidi ya hayo, Ulaya ni lazima ipate uungaji mkono wa China katika kudumisha anuai ya baiolojia, operesheni za ulinzi wa amani duniani, kusuluhisha migogoro, kuondokana na umasikini duniani na majadiliano ndani ya taasisi za pande nyingi kama vile Umoja wa Mataifa.

Ingawa uhusiano kati ya China na Ulaya unaanza kufufuka kwa taratibu, baadhi ya migongano ya kimfumo kati ya pande hizo mbili haiwezi kupuuzwa. Kutokana na kuongezeka kwa ufahamu wa siasa za kijiografia, Umoja wa Ulaya na baadhi ya nchi wanachama wake wanaweza kuchukua msimamo mkali dhidi ya China katika masuala ya haki za binadamu na siasa. Pia, chini ya mtazamo wa kupunguza hatari, hatua ya Ulaya kujitenga na China katika teknolojia na biashara inaweza kuendelea kuongezeka. Zaidi ya hayo, kutokana na mchezo mkubwa wa nguvu kati ya China na Marekani, kuimarisha uhusiano wa ng’ambo ya bahari ya atlantiki kutasababisha shinikizo zaidi la Marekani kwa Ulaya.

Kutokana na hayo yote, umefika wakati ambao Ulaya inaihitaji zaidi China. Pia, kama pande mbili kubwa zenye nguvu, maendeleo mazuri ya uhusiano wa China na Umoja wa Ulaya sio tu yanaendana na maslahi ya maendeleo ya kiuchumi ya pande hizo, bali pia ni muhimu katika kuleta uaminifu kwenye dunia inayokabiliwa na migogoro na zintofahamu, na kusaifia kufufuka kwa uchumi wa dunia, na kudumisha amani ya dunia.