Kongamano la kutangaza maonesho ya China na Afrika la Kenya lasifu maonesho hayo kutoa jukwaa la kubadilishana mafunzo juu ya ukuaji
2023-05-15 08:52:32| CRI

Maonesho ya tatu ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika yanatoa jukwaa la kuvutia uwekezaji na kubadilishana maarifa ambayo yanaweza kuchochea ukuaji wa Afrika.

Akiongea kando ya kongamano la kutangaza maonesho hayo lililofanyika mjini Nairobi, Kenya, afisa mkuu mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda nchini Kenya (KNCCI) Patrick Nyangweso, alisema maonesho hayo ni muhimu kwa uchumi wa Afrika kufuatia juhudi za kutafuta masoko mapya, mtiririko wa mitaji na ubunifu kutoka China ili kufufua sekta muhimu, kama vile viwanda, usindikaji wa kilimo, na uchumi wa kidijitali.

Maonesho hayo ya tatu yenye kauli mbiu "Maendeleo ya Pamoja kwa Mustakabali wa Pamoja," yataanza Juni 29 hadi Julai 2 katika Mkoa wa Hunan, China. Yakizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2019, maonesho haya ni jukwaa kuu la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Afrika.

Akihudhuria kwenye kongamano hilo Naibu meya wa Yiyang, Yang Zhihua, alisema maonesho hayo yatakayojumuisha semina, mazungumzo ya biashara, na mabanda ya bidhaa za nje yatahitimishwa kwa kutolewa kwa kielelezo cha biashara kati ya China na Afrika.