Mapigano yaendelea kati ya pande hasimu za Sudan katika mji mkuu Khartoum
2023-05-16 08:45:59| CRI

Mapigano kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) yaliendelea siku ya Jumatatu, huku maeneo ya mashariki ya mji mkuu Khartoum yakishuhudia mashambulizi makali ya jeshi la anga.

Kwenye taarifa yake Jeshi la Sudan limesema usambazaji mkubwa wa vifaa vya silaha, risasi na mafuta ya wanamgambo waasi umeshughulikiwa katika operesheni kubwa ambayo ililenga baadhi ya maeneo ya Sharq Al-Neel (mashariki mwa Nile) na kambi karibu na Hospitali ya Nile Mashariki.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa hakukuwa na majeruhi ya raia wakati wa operesheni hiyo, lakini RSF ilisema shambulio hilo la bomu lilisababisha vifo na majeruhi ya makumi ya raia wasio na hatia na uharibifu wa sehemu kubwa ya hospitali.

Pia siku ya Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ililaani kile ilichokiita "mashambulizi ya RSF" kwenye balozi kadhaa za mjini Khartoum.

Wakati huo huo, Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu nchini Sudan Jumatatu ilitoa taarifa ikilaani matumizi ya vikosi vya anga na silaha nzito karibu na makazi ya raia, ambayo yalisababisha vifo vya raia.