Marais wa China na Eritrea wafanya mazungumzo
2023-05-16 08:54:04| CRI

Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Eritrea Isaias Afwerki ambaye yupo ziarani nchini China wamefanya mazungumzo siku ya Jumatatu katika Jumba la Mikutano ya Umma la China mjini Beijing. Rais Xi ameeleza kuwa, China inapenda kuimarisha uhusiano wa kirafiki na kindugu kati yake na Eritrea, na kuhimiza uhusiano wa kiwenzi na wa kimkakati kati ya pande hizo mbili kupata maendeleo katika kiwango kipya.

Katika mazungumzo hayo, Rais Xi amesisitiza kuwa China inapenda kushirikiana na Eritrea kuhimiza ushirikiano wa kunufaishana kupitia ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika na “Wazo la Maendeleo ya Amani la Pembe ya Afrika”, ili kupata maendeleo ya pamoja.

Naye rais Afwerki ameeleza kuwa Eritrea ina matumaini ya kuimarisha ushirikiano na China, na kuamini kuwa uhusiano wa kiwenzi na kimkakati kati ya pande hizo mbili utachangia katika kutimiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo.