IOM yaomba tena dola milioni 58.5 kusaidia wahamiaji wa Pembe ya Afrika
2023-05-16 08:44:35| CRI

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) Jumatatu liliomba tena dola za kimarekani milioni 58.5 ili kutoa msaada wa kibinadamu kwa ajili ya kuokoa maisha ya zaidi ya wahamiaji milioni 1 walio hatarini katika "Njia ya Mashariki," ambayo inaanzia katika Pembe ya Afrika hadi Yemen na mataifa ya Ghuba.

Kwenye taarifa yake IOM limesema uhaba wa fedha unasababisha kukosekana kabisa kwa misaada ya kibinadamu na ulinzi kwa wahamiaji, ukiwemo msaada unaotolewa katika vituo vya kuhudumia wahamiaji kwenye njia hiyo.

Mwezi Februari, IOM na washirika wake 47 wa kibinadamu na maendeleo waliomba dola milioni 84.2 lakini hadi sasa zimetolewa dola milioni 2 tu. Kwa mujibu wa IOM, "Njia ya Mashariki" ni mojawapo ya njia hatari na ngumu zaidi za uhamaji wa binadamu barani Afrika na duniani.

Mamia kwa maelfu ya watu hasa kutoka Ethiopia na Somalia husafiri kwa njia hiyo kila mwaka wakitarajia kufika nchi za Ghuba kutafuta kazi na kukabiliwa na hatari za kutishia maisha yao zikiwemo njaa na upungufu wa maji mwilini.