Mkoa wa Plateau nchini Nigeria waweka marufuku ya kutotoka nje baada ya watu kadhaa kuuawa katika shambulio
2023-05-17 22:26:00| cri

Serikali ya mkoa wa Plateau, katikati ya Nigeria, imeweka marufuku ya kutotoka nje kwa saa 24 katika vijiji vya Fungzai na Kubat vilivyoko eneo la Mangu mkoani humo baada ya watu wenye silaha kushambulia vijiji viwili jirani na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Gavana wa Mkoa huo Simon Lalong amesema katika taarifa yake kuwa, mashambulio hayo yalitokea jumatatu usiku, na kuyaelezea kuwa ni ya kusikitisha, ambapo kati ya watu waliouawa, ni wanawake na watoto.

Hakuna idadi kamili ya vifo iliyotolewa rasmi, lakini vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti kuwa zaidi ya watu 20 wameuawa katika mashambulio hayo.

Mashambulio ya silaha yamekuwa tishio kubwa la kiusalama katika maeneo ya kaskazini na katikati ya Nigeria, ambayo yamesababisha vifo na utekaji nyara katika miezi ya karibuni.