Rais wa China atoa agizo kuhusu ajali ya kupinduka kwa meli ya uvuvi ya China kwenye bahari ya Hindi
2023-05-17 14:24:55| cri

Meli ya uvuvi ya baharini inayomilikiwa na kampuni ya uvuvi ya Penglaijinglu ya China ilipinduka na kuzama katika sehemu ya katikati ya bahari ya Hindi.

Watu 39 waliokuwa ndani ya meli hiyo bado hawajajulikani walipo wakiwemo mabaharia 17 wenye uraia wa China, raia 17 wa Indonesia na raia watano wa Ufilipino, na kazi ya uokoaji bado inaendelea.

Baada ya ajali hiyo kutokea, rais Xi Jinping wa China ameagiza Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Vijiji, Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, na serikali ya mkoa wa Shandong kutekeleza mara moja utaratibu wa mwitikio wa dharura, kuthibitisha hali halisi, kuongeza nguvu ya uokoaji, kuratibu misaada ya kimataifa ya utafutaji na uokoaji baharini na kufanya juhudi zote za uokoaji.

Wakati huohuo, Rais Xi pia ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje ya China na Ubalozi wa China katika nchi zinazohusika kuimarisha mawasiliano na mamlaka husika za nchi hizo, ili kuratibu kazi za uokoaji. Aidha, idara husika za ndani zinatakiwa kuimarisha zaidi hatua za kukagua na kutambua hatari za usalama wa uvuvi wa baharini na kutoa tahadhari za mapema, ili kuhakikisha usalama wa maisha na mali za wananchi.