Rais Xi Jinping akutana na mwenzake wa Kyrgyzstan mjini Xi’an
2023-05-18 14:42:49| cri

Rais Xi Jinping wa China leo asubuhi amekutana na mwenzake wa Kyrgyzstan Sadyr Japarov ambaye yuko ziarani nchini China na kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa China na Asia ya Kati mjini Xi’an. Wakuu wa nchi hizo mbili wametangaza kuinua uhusiano wa nchi zao hadi kufikia ngazi ya Uhusiano wa Wenzi wa Kimkakati wa Pande Zote katika Zama Mpya.

Kwenye mazungumzo hayo, Rais Xi amesema makubaliano yaliyofikiwa kati yao mwaka jana kuhusu uhusiano wa pande mbili na ushirikiano katika nyanja mbalimbali yamekuwa yakitekelezwa kwa ufanisi na kutia msukumo mkubwa kwenye maendeleo ya uhusiano wa nchi hizo mbili, ambao umetimia miaka 31. Amesema China inapenda kushirikiana na Kyrgyzstan katika kujenga jumuiya yenye mustakabali wa  pamoja, ujirani mwema na ustawi wa kunufaishana kati ya China na Kyrgyzstan, ili kuchangia maendeleo na ustawi wa nchi zote mbili.

Kwa upande wake, Rais Japarov amesema, hivi sasa uhusiano kati ya Kyrgyzstan na China uko kwenye kiwango cha juu katika historia, msimamo wa nchi yake wa kuiunga mkono China kwenye masuala yanayohusiana na maslahi yake makuu  kuhusu Taiwan, Xinjiang na Hongkong, ni thabiti na hautabadilika, na Kyrgyzstan inapenda kuungana mkono kithabiti na upande wa China, na kuimarisha mawasiliano na uratibu, ili kuhimiza kwa pamoja usalama na maendeleo ya nchi hizo mbili na kanda nzima.