Serikali na jumuiya ya wafanyabiashara ya Rwanda watashiriki katika Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) yatakayofanyika mjini Shanghai mwezi Novemba, kwa lengo la kupata ushirikiano muhimu wa kibiashara na makampuni ya China.
Nelly Mukazayire, naibu afisa mkuu mtendaji wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB), alitoa tangazo hilo katika mkutano wa kutangaza maonesho ya CIIE uliofanyika Kigali, Rwanda siku ya Jumatano.
Mukazayire amesisitiza kuwa maonesho ya CIIE yanatoa jukwaa bora la kufanya chapa za bidhaa za Rwanda zitambuliwe zaidi na kuvutia wawekezaji wa China. Alisema mwaka huu Rwanda itakuwa inashiriki mara ya sita kwenye maonesho ya CIIE, na ushiriki wake endelevu umeongeza kwa kiasi kikubwa uelewa wa bidhaa za Rwanda katika soko la China.
Naye Song Shangzhe, naibu mkurugenzi mkuu wa Ofisi ya Maonesho ya Kimataifa ya Uagizaji ya China ambaye yuko ziarani nchini humo, alieleza nia ya dhati ya China kuipatia soko lake Rwanda na dunia kupitia maonesho hayo. Alisisitiza matokeo chanya ya CIIE kwenye ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Rwanda na kuwezesha makampuni ya Rwanda kupata soko kubwa la China.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Rwanda Wang Xuekun alisisitiza kuwa CIIE si maonesho ya wiki moja tu bali pia ni jukwaa la kiuchumi ambapo watu mashuhuri, maafisa wa kimataifa na wasomi hukusanyika ili kujadili ushirikiano wa kiuchumi.