Marais wa China na Kazakhstan wafanya mazungumzo
2023-05-18 08:57:41| CRI

Rais Xi Jinping wa China amefanya mazungumzo na mwenzake wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev ambaye yupo ziarani nchini China na kushiriki kwenye Mkutano wa Viongozi kati ya China na Asia ya Kati jana Jumatano mjini Xi’an.

Katika mazungumzo hayo, rais Xi amesema China na Kazakhstan ziko katika kipindi muhimu cha kupata maendeleo na ustawi. China inaunga mkono kithabiti Kazakhstan kulinda uhuru, mamlaka na ukamilifu wa ardhi, na kuiunga mkono ijiendeleze kwa kufuata hali yake yenyewe.

Kwa upande wake Tokayev ameeleza kuwa, Kazakhstan inapenda kushirikiana na China, kuimarisha uhusiano wa kudumu wa kiwenzi na kimkakati wa pande zote, kupanua ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika sekta za biashara, utalii na utamaduni, ili kuweka msingi thabiti kwa ajili ya kufungua Miongo Mipya Mitatu Bora kati ya pande hizo mbili.